IQNA

Baraza la Haki za Binadamu UN lataka mauaji ya Khashoggi yachunguzwe

16:25 - December 05, 2018
Habari ID: 3471762
TEHRAN (IQNA)- Kamishna MKuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kubaini mhusika wa mauaji ya mwandishi habari Msaudi Jamal Khashoggi.

Akizungumza Jumatano katika mkutano wa waandishi habari mjini Geneva, Bachelete amesema kuna haja ya uchunguzi wa kimataifa kuhusu mauaji ya Khashoggi ili kubaini wahusika wakuu wa mauaji hayo ya kinyama.

Siku ya Jumatano pia Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Isttanbul Uturuki alisema ametoa waranti wa kukamatwa mpambe mkuu wa Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mohammad bin Salman na naibu mkuu wa Ujasusi wa Kigeni Saudia kwa kushukiwa kuwa wahusika wakuu wa mauaji ya Khashoggi. Mwendesha Mashttaka MKuu wa Istanbul amesema kuna uwezekano mkubwa kuwa watu hao wawili ambao wametajwa kuwa ni Saud al-Qahtani na Jenerali Ahmed al-Asiri, ambao waliondolewa katika nafasi zai mwezi Okotba walikuwa wapangaji wakuu wa mauaji ya Khashoggi.

Wakati huo huo Seneta mashuhuri wa Marekani Lindsey Graham amekosoa vikali siasa za Saudi Arabia na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman na kusisitiza kuwa, Kongresi ya Marekani itachukua msimamo mkali ili kukomesha sera mbovu za Riyadh bila ya kujali msimamo wa serikali ya Rais Donald Trump.

Lindsey Graham amesema kwamba, mauaji yaliyofanywa na utawala wa Saudi Arabia dhidi ya mwandishi na mkosoaji wa nchi hiyo, Jamal Khashoggi, mashambulizi na uvamizi wa nchi hiyo huko Yemen, kuizingira Qatar na jaribio la Saudia la kutaka kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad al Hariri yote hayo ni kielelezo cha sera za kijuba na ukiukaji wa sharia za kimataifa.

Jamal Khashoggi, aliyewahi kuwa msiri na mwandani wa familia ya kifalme inayotawala nchini Saudi Arabia, aligeuka na kuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud. Jamal aliuliwa tarehe Pili Oktoba mwaka huu na timu ya mauaji iliyotumwa Istanbul Uturuki na Muhammad bin Salman baada ya kuingia kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo na mwili wake ukakatwa vipande vipande.    

3467392

captcha