IQNA

Rais Rouhani katika ujumbe wa Nowruz

Taifa la Iran kwa yakini litapata ushindi

9:46 - March 21, 2019
Habari ID: 3471883
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mapema Alhamisi ametuma ujumbe kwa kunasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1398 Hijria Shamsiya na kusema mwaka 1397 ulikuwa mwaka wa mafanikio makubwa ya taifa la Iran katika nyuga mbali mbali na kuongeza kuwa, kwa yakini taifa la Iran litapata ushindi na litavuka matatizo yaliyopo.

Rais Rouhani ameashiria vikwazo vya upande mmoja na vilivyo kinyume cha sheria vya Marekani dhidi ya taifa la Iran na kusema: "Adui alifikiri kuwa dunia nzima ingesimama pamoja  naye katika vikwazo hivyo, lakini isipokuwa nchi chache tu, nchi zote duniani zimesimama na taifa la Iran."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kusema kuwa, taasisi zote za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki zimethibitisha kuwa taifa la Iran limesimama katika haki. Ameongeza kuwa, wale ambao wamevunja ahadi zao na kufanya khiana  wanapaswa kufahamu kuwa mwisho hautakuwa kwa maslahi yao.

Rais Rouhani pia ameashiria uhusiano mzuri wa Iran na nchi za eneo na kusema: "Mwaka mpya ni mwaka wa urafiki zaidi na majirani wote."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelihutubia taifa kubwa la Iran na kusema mwaka mpya ni mwaka wa mshikamano zaidi na jitihada zaidi.

Rouhani ameongeza kuwa, katika mwaka mpya, Wiarani watashikana na kuwa kitu kimoja na wataonyesha izza na adhama yao katika kukabiliana na wale wanaotaka kulivunja taifa hili.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mwaka mpya ni mwaka wa kuimarisha uzalishaji bidhaa ndani ya nchi kwa lengo la kubuni nafasi za ajira kwa vijana. Amesema serikali itatumia uwezo wake wote kufanikisha jambo hilo.

Kwa munasaba wa mwaka mpya wa Hijria Shamsia, Rais Rouhani ametuma salamu za kheri na fanaka kwa taifa kubwa la Iran, Wairani waishio nje ya nchi na kwa kaumu na nchi jirani ambazo huadhimisha Nowruz.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka mpya wa 1398 Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani inajulikana kama Sikukuu ya Nowruz au Nairuzi kwa wanaozungumza Kiswahili.. Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni kama Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi Machi 21 (yaani tarehe Mosi Farvardin) kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.

3799266

captcha