IQNA

UAE yaondoa askari wake Yemen na kutoa pigo kwa Saudia Arabia

23:24 - July 12, 2019
Habari ID: 3472040
TEHRAN (IQNA) - Watawala wa Saudi Arabia wamekasirishwa na kitendo cha Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) cha kuwaondosha nchini Yemen idadi kubwa ya wanajeshi wake.

Duru kadhaa za kidiplomasia zimedokeza kuwa uamuzi huo wa UAE haujawakasirisha tu watawala wa Saudia, bali pia kimetoa pigo kubwa kwa madola ya Magharibi.
Taarifa zinasema UAE imechukua hatua ya kupunguza idadi kubwa ya askari wake kutokana na kulemewa na gharama kubwa ya vita dhidi ya Wayemen, na kwa mantiki hiyo imeamua kuchukua uamuzi huo bila kujali iwapo itaghadhabisha muitifaki wake, Saudia.
Wanadiplomasia wanne wamenukuliwa na shirika la habari la Reuters wakisema kuwa, UAE imelazimika kupunguza idadi ya wanajeshi wake baada ya kuongezeka wasiwasi wa kutokea vita katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
Hata hivyo baadhi ya duru za habari zimedokeza kuwa, Abu Dhabi imechukua uamuzi huo baada ya kushuhudia wimbi la vipigo kutoka kwa vikosi vya jeshi la Yemen vikisihirikiana na kamati za wananchi.
Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, Umoja wa Falme za Kiarabu umeripotiwa kupunguza karibu asilimia 80 ya wanajeshi wake kutoka mji wa bandari wa al-Hudaydah huko kusini mwa Yemen.
Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ikishirikiana na UAE zilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasiopungua 16,000 wasio na hatia. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha katika vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani, Uingereza na utawala haramu wa Israel. Hivi karibuni Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Watoto, Save The Children, lilitangaza kuwa watoto zaidi ya 84,700 wa Yemen wamepoteza maisha kutokana na makali ya njaa na utapiamlo, tangu Saudi Arabia ianzishe vita dhidi ya nchi hiyo maskini jirani yake zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, ripoti mbalimbali za Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) zimekuwa zikitahadharisha kuhusiana na matokeo mabaya na maafa yanayosababishwa na kuendelea hujuma ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake huko nchini Yemen.
Aidha ripoti mbalimbali zinaeleza kwamba, zaidi ya watoto milioni 11 wa Yemen wanakabiliwa na uhaba wa chakula, maradhi na ukosefu wa makazi.

3468934

captcha