IQNA

Matukio ya Afghanistan

Wasiwasi wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali mbaya ya kimaisha Afghanistan

18:13 - September 10, 2021
Habari ID: 3474280
TEHRAN (IQNA)- Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, asilimia 97 ya wananchi wa Afghanistan wamo katika hatari ya kuingia chini ya mstari wa umasikini.

Sambamba na indhari yake hiyo, Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuongezwa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wananchi wa Afghanistan.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, endapo matakwa ya kusaidiwa wananchi wa Afghanistan kwa ajili ya kukabiliana na mgogoro wa kisiasa na kiuchumi hayatafanyiwa kazi, basi asilimia 97 ya wananchi hao watakuwa katika hatari ya kutumbukia chini ya mstari wa umasikini.

Ripoti hiyo inatolewa siku chache tu baada ya Martin Griffiths Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu kutangaza kuwa, nusu ya wananchi wa Afghanistan wanahitajia misaada ya haraka ya kibinadamu.

Hivi karibuni pia, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, (OCHA) ilitangaza kuwa, mamilioni ya wananchi wa Afghanistan wanahitajia misaada ya chakula pamoja na huduma za kiafya na kwamba, kwa sasa sekta ya utoaji huduma nchini Afghanistan inakabiliwa na hali mbaya na imo katika hatua ya kusambaratika.

Mwezi uliopita wa Agosti serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghani ilisambaratika na kiongozi huyo kuikimbia nchi baada ya Taliban kuingia Kabul mji mkuu wa Afghanistan. Wachambuzi wa mambo wanasema, hatua ya Taliban ya kuudhibiti mji wa Kabul imehitimisha uvamizi wa miaka 20 wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa kisingizio cha kuijenga upya Afghanistan.

Wito wa kiongozi wa Taliban

Hibatullah Akhundzada kiongozi mkuu wa kundi la wanamgambo wa Taliban amewataka wananchi wa Afghanistan kuiunga mkono serikali ya mpito ya kundi hilo. Amesema, Afghanistan ni nyumba ya taifa lote la Afghanistan na kwamba nyumba hiyo ni muhimu katika kuijenga nchi.

Malalamiko na maandamano ya wananchi wa Afghanistan yanaonyesha kuwa, hatua za kundi la Taliban katika karibu siku 20 zilizopita tangu kundi hilo lilipoudhibiti mji wa Kabul zimeshindwa kuwashawishi raia wa nchi hiyo na zimesababisha wasiwasi katika duru za kieneo na kimataifa.

Iran yasistiza usalama wa Afghanistan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, suala la usalama na utulivu wa Afghanistan ni muhimu sana kwa Iran.

Hossein Amir-Abdollahian ameandika hayo na kuongeza kuwa, suala la usalama, utulivu na ustawi wa Afghanistan limejadiliwa pia katika kikao kilichofanyika kwa njia ya Intaneti, cha nchi sita zinazopakana na nchi hiyo. 

Aidha ameandika: Katika kikao hicho, kulihimizwa kuundwa serikali kubwa ya watu wa matabaka yote itakayoridhiwa na jamii ya Waafghani, kutilia mkazo mazungumzo na kujiweka mbali na machafuko, utumiaji nguvu na uingiliaji wa kigeni.

Kikao cha nchi sita zinazopakana na Afghanistan kilifanyika kwa njia ya Intaneti jana Jumatano. Nchi zilizoshiriki kwenye kikao hicho ni Iran, China, Pakistan, Uzbekistan, Tajikistan na Turkmenistan. 

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abdullah bin Zayed Al Nahyan, Jumatano alifanya mazungumzo ya simu na Bw. Hossein Amir-Abdollahian. Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Pande hizo mbili zimetilia mkazo wajibu wa kuimarishwa uhusiano wao zikiwa ni nchi jirani ambazo kila moja inamuhitajia mwenzake, kama ambavyo zimejadiliana pia masuala ya kieneo na kimataifa.

Katika mazungumzo hayo, Bw. Abdollahian amegusia mazungumzo yake ya hivi karibuni na Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mohammed bin Rashid Al Maktoum na jinsi pande mbili zilivyo na mitazamo chanya kuhusu ushirikiano baina yao katika masuala mbalimbali yakiwemo ya ustawi.

 

3996425

captcha