IQNA

Yale ambayo yamejiri miaka 20 baada ya mashambulizi ya Septemba 11

20:57 - September 11, 2021
Habari ID: 3474282
TEHRAN (IQNA)- Miaka 20 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 11 Septemba mwaka 2001, ndege mbili kati ya nne za abiria za Marekani zilizotekwa nyara ziligonga minara miwili pacha ya jengo la Biashara la Kimataifa la mjini New York huku ndege moja ikigonga jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington.

Ndege ya nne ililengwa ikiwa katika anga ya Pensylvania na kuangushwa. Baadhi ya ghorofa za jengo la Biashara ya Kimataifa ziliporomoka na sehemu ya jengo la Pentagon pia ikaharibiwa katika mashambulizi hayo ya kigaidi. Karibu watu 3200 waliuawa katika mashambulizi hayo. Marekani ilitangaza kuwa mtandao wa al Qaida uliokuwa ukiongozwa na Usama bin Laden raia wa Saudi Arabia, ndio uliohusika na mashambulizi hayo. Baada ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani, kulianza wimbi la ubaguzi na mashambulizi dhidi ya Waislamu na matukufu ya dini yao katika nchi za Magharibi.

Taarifa ya Biden

Jana ikiwa imebakia siku moja kabla ya kutimia mwaka wa 20 tangu baada ya mashambulizi ya Septemba 11 ambayo yaliua watu karibu elfu tatu, Rais Joe Biden wa Marekani alitoa ujumbe akitaka kuwepo umoja na mshikamano wa kitaifa nchini Marekani.

Biden alisema, umoja wa kitaifa ndilo somo kubwa zaidi la mashambulizi ya Septemba 11 kwa jamii yenye watu wa mbari na kaumu tofauti ya Marekani. Amesisitiza kuwa, maana ya umoja si watu wote kuamini kitu kimoja, bali kwa maana ya taifa moja kuheshimiana na kuaminiana.

White House imerusha hewani ujumbe huo kabla ya shughuli ya kukumbuka tukio la Septemba 11 ambayo mwaka huu inafanyika huku Marekani ikiwa bado inasumbuliwa na athari mbaya za mashambulizi hayo ambayo tunaweza kusema kuwa, yalianzisha kipindi na awamu mpya katika mahusiano ya kimataifa. Mashambulizi hayo pia ni tukio lililokuwa na taathira kubwa katika siasa za nje za Marekani. Baada ya mashambulizi hayo, rais wa zamani wa Marekani, Goerge W. Bush alikhitari siasa na sera za kuhujumu nchi mbalimbali kwa kisingizio cha mapambano ya kimataifa dhidi ya ugaidi. Zaidi ya watu milioni moja wameuawa katika nchi za Iraq, Afghanistan, Syria, Libya na Yemen katika vita hivyo vya Marekani eti 'dhidi ya ugaidi'. 

Matukio ya Afghanistan

Katika upande mwingine, mwaka wa 20 wa tangu tukio la Septemba 11 umesadifiana na tukio la kuondoka kwa madhila majeshi ya Marekani na NATO huko Afghanistan. Baada ya vita na uvamizi wa miaka 20 dhidi ya Afghanistan kwa kile kilichotajwa kuwa ni kuangamiza makundi ya Taliban na al Qaida, Marekani imelazimika kuondoka nchini humo kwa fedheha kubwa ya kisiasa na kijeshi na bila ya mafanikio ya aina yoyote. Kuondoka huko sambamba na kundi la Taliban kuchukua tena udhibiti wa Afghanistan, kumeifanya serikali ya Joe Biden ikosolewe sana ndani na nje ya Marekani.

Kubaguliwa Waislamu

Suala jingine linalopaswa kuashiria ni mchango wa tukio la Septemba 11 katika kuchochea chuki na propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Marekani. Uchunguzi unaonesha kuwa, vita na propaganda chafu zimeongezeka sana nchini Marekani na Magharibi kwa ujumla katika kipindi cha miaka 20 iliyopita baada ya mashambulizi ya Septemba 11. Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na taasisi ya PEW unaonesha kuwa, asilimia 82 ya Wamarekani wanaamini kuwa Waislamu wanabaguliwa. Idadi kubwa ya Waislamu wa Marekani wanahisi kwamba, wanahukumiwa kwa kosa ambalo hawakulitenda wala kuliunga mkono. Vita na propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu vilishadidi zaidi kipindi cha utawala wa Donald Trump ambaye aliunga mkono waziwazi misimamo ya kufurutu mipaka ya mrengo wa kulia. Trump alizidisha mashambulizi dhidi ya Waislamu kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Alikwenda mbali zaidi na kutoa dikrii ya kuwazuia raia wa nchi sita za Waislamu kuingia Marekani na akawataja Waislamu kuwa ni magaidi. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, serikali ya Marekani yenyewe imechochea ukatili na propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu. Hivyo basi, wito wa Joe Biden wa kuwepo umoja na mashikamano wa kitaifa unatazamwa kwa jicho la shaka na maswali mengi yasiyokuwa na majibu, ila tu iwapo tutawatambua Waislamu Wamarekani kuwa si raia wa Marekani!

Kuhusika Saudia katika hujuma za 9/11

Nukta nyingine inayojadiliwa kuhusiana na tukio la Septemba 11 ni jitihada zinazofanywa na serikali za Marekani kuanzia utawala wa George W. Bush hadi Donald Trump za kuficha nafasi ya Saudi Arabia katika mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 kwa kusingizio kwamba kufuatiliwa suala hilo kutakua na taathira hasi kwa uhusiano wa Washington na Riyadh. Sababu ya kuukingia kifua utawala wa kifalme wa Saudia ni maslahi ya kiuchumi na kistratijia ya Marekani na nafasi ya serikali ya Saudia katika kulinda maslahi ya Washington katika eneo la Magharibi mwa Asia. Serikali ya Biden pia japokuwa awali ilijifanya kuchukua misimamo mikali kuhusiana na Saudi Arabia na kudai kuwa itatazama upya uhusiano wake na Riyadh, lakini hatimaye imeimarisha uhusiano mkubwa na mpana na Riyadh kwa kile kinachodaiwa ni kutilia maanani maslahi ya Washington na masuala ya kistratijia!    

Kwa sasa mashinikizo ya familia za wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 yamemlazimisha Joe Biden atoe amri ya kufichuliwa na kuwekwa wazi nafasi ya viongozi wa serikali ya Saudi Arabia katika mashambulizi hayo. 

3996388/

captcha