IQNA

Nasrallah: Imam Khomeini (MA) alileta umoja katika ya Waislamu Shia na Sunni

18:51 - October 23, 2021
Habari ID: 3474462
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuhusu mchango usio na kifani wa Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Amrehemu-MA-) wa kuleta umoja kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Sunni.

Sayyid Hassan Nasrallah ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa usiku wa kuamkia leo kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad (SAW).

Sambamba na kutoa mkono wa pongezi na wa kheri na baraka kwa mazazi ya Bwana Mtume Muhammad Al-Mustafa (SAW) na Imam Jaafar Sadiq (AS) na kuwadia maadhimisho ya Wiki ya Umoja, Sayyid Hassan Nasrallah amesema, miongoni mwa baraka za hatua alizochukua Imam Khomeini (MA) na matunda ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yalikuwa ni suala wanalotafautiana Waislamu la tarehe ya kuzaliwa Mtume (SAW) kuwa nukta ya kuwaunganisha na kupatikana umoja baina yao.

Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaitambua tarehe 12 Mfunguo Sita, Rabiul-Awwal kuwa ndio siku aliyozaliwa Bwana Mtume Muhammad (SAW), wakati kwa mtazamo wa Waislamu wa madhehebu ya Shia siku ya kuzaliwa Nabii huyo wa rehma ni tarehe 17 ya mwezi huo.

Imam Khomeini (MA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambaye yeye mwenyewe alikuwa miongoni mwa walinganiaji wa umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu, alilitumia suala hilo kwa ajili ya kuwaleta karibu na kuwaunganisha Waislamu; na akatangaza kuwa, kipindi cha baina ya tarehe mbili hizo (12 hadi 17 Rabiul-Awwal) ni "Wiki ya Umoja".

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amezungumzia pia mateso na machungu wanayopata wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na akaeleza kwamba, hakuna mtu yeyote aliyekomboka kifikra awezaye kuipuuza Palestina, watu wake wanaodhulumiwa na matukufu yake.

Sayyid Hassan Nasrallah ameashiria pia jinai za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen na akaitaka jamii ya kimataifa badala ya kuwalaani wanaoathirika kwa jinai hizo nchini Yemen isikilize kilio na matakwa ya mamilioni ya watu wa Yemen.

4007167/

captcha