IQNA

Vita dhidi ya ugaidi

Mwanzilishi mwenza wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab ameuawa

23:13 - October 03, 2022
Habari ID: 3475873
TEHRAN (IQNA) – Mmoja wa waanzilishi wenza wa kundi la kigaidi la al-Shabaab, Abdullahi Nadir, ameuawa katika operesheni ya pamoja ya kijeshi mwishoni mwa juma, serikali ya Somalia ilisema.

Haya yanajiri huku magaidi hao wakidai kuhusika na shambulio jipya siku ya Jumatatu.

Vikosi vya usalama vya Somalia vimesema kumepatikana mafanikio makubwa katika wiki za hivi karibuni dhidi ya kundi hilo la kigaidi lenye uhusiano na al Qaeda. Mafanikio hayo yamepatikana kupitia msaada wa  vikundi vya kujilinda vya ndani ya nchi.

Lakini al Shabaab wameendelea kufanya mashambulizi mabaya, yakiwemo mawili ya Ijumaa iliyopita yaliyoua takriban watu 16 na jingine Jumatatu ambalo polisi walisema liliua watu wasiopungua watano.

Wizara ya habari ya Somalia ilisema katika taarifa yake Jumapili jioni kwamba operesheni iliyomuua Nadir ilifanyika Jumamosi. Taarifa zinadokeza kuwa, Nadir pia alikuwa mwendesha mashtaka mkuu wa magaidi wa al-Shabaab na alikuwa katika mstari wa kuchukua nafasi ya kiongozi wa kundi hilo, Ahmed Diriye, ambaye ni mgonjwa.

"Kifo chake ni mwiba ulioondolewa kutoka kwa taifa la Somalia," taarifa ya serikali ya Somalia imesema. "Serikali inawashukuru watu wa Somalia na marafiki wa kimataifa ambao ushirikiano wao uliwezesha kuuawa kwa kiongozi huyu ambaye alikuwa adui wa taifa la Somalia."

Al-Shabaab hawajatoa maoni kuhusu kifo cha Nadir.

Magaidi wa Al-Shabaab wameua makumi ya maelfu ya watu katika mashambulizi ya mabomu tangu mwaka 2006 katika vita vyao vya kupindua serikali kuu ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, aliyechaguliwa na wabunge mwezi Mei, ameahidi kukabiliana na magaidi wa al Shabab.

Katika shambulio la al-Shabaab siku ya Jumatatu, magari mawili yaliyotegwa mabomu katika mji wa kati wa Beledweyne yaliua takriban watu watano wakiwemo wanajeshi na maafisa wa eneo hilo.

Alipoulizwa maoni yake, msemaji wa operesheni za kijeshi wa al-Shabaab alisema kundi lilitekeleza shambulio la Beledweyne, ambapo alidai kuwa makumi ya watu, wakiwemo maafisa na wanajeshi, wameuawa.

3480711

captcha