IQNA

Hafidh wa Qur'ani kutoka Nigeria

'Nyumba yangu ni Madrassah ya Qur'ani'

14:36 - May 21, 2015
Habari ID: 3306135
'Nyumba yangu ni Madrassah ya Qur'ani na tokea utotoni nimekuwa nikijifunza Qur'ani na nilianza kuihifadhi nikiwa na umri wa miaka 14' anasema Hafidh wa Qur'ani kutoka nchini Nigeria.

Mohammad Barnamah Mahmoud  mwakilishi wa Nigeria katika Awamu ya 32 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran katika mahojiano maalumu na Shirika la Kimataifa la Habari la Qur'an la Iran IQNA amesema: "Tukiangazia ukumbi wa mashindano tunaona watu wa madhehebu mbali mbali za Kiislamu na wote wamedhihirisha ukarimu na mapenzi. Qur'ani Tukufu tu ndiyo inayoweza kuwaleta Waislamu namna hii. Kwa msingio huo tunapaswa kurejea kikamilifu katika Qur'ani Tukufu huku tukishikamana na kuimarisha umoja wetu."
Mohammad Mahmoud ambaye ni mwanachuo wa Shahada ya Uzamili (MA) katika Tafsiri ya Qur'ani katika Chuo Kikuu cha Kano kaskazini mwa Nigeria anasema katika nyumba yake anatoa mafundisho ya Qur'ani kwa watoto na mabarobaro.
Anasema mwaka 2006 alishiriki katika mashindano ya Qur'ani nchini Malaysia na mwaka 2009 nchini Saudi Arabia ambapo alipata nafasi ya tatu katika tafsiri ya Qur'ani. Hafidh Mohammad Mahmoud anasema hii ndio mara ya kwanza  kwake kushiriki katika mashindano ya Qur'ani nchini Iran. Anaamini kuwa mashindano ya Qur'ani ya Iran yakifuatiwa na ya Malaysia na kisha ya Dubai ndio bora zaidi katika kiwango cha kimataifa. Hafidh huyo wa Qur'ani mwenye umari wa miaka 27 anasema baba yake na ndugu zake pia ni waalimu wa Qur'ani Tukufu.

Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yalianzanza sambamba  na mnasaba wa Mab’ath (kubaathiwa  au kupewa utume Mtume Muhammad- SAW-), Tarehe 27 Rajab.  Mashindano hayo ya kila mwaka yataendelea kwa muda wa wiki moja hadi Ijumaa tarehe 22.
Wasomi (maqarii) na waliohifadhi Qur’ani kikamilifu kutoka nchi za Kiislamu na zisizo na Kiislamu watashiriki katika mashindano hayo ya wiki moja.../mh

3305869

captcha