IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mpango jumla wa adui umefeli kwani irada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa imara zaidi

20:07 - January 12, 2023
Habari ID: 3476390
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mpango jumla wa adui umegonga mwamba kwa sababu mahesabu yao yalikuwa ghalati na irada ya Jamhuri ya Kiislamu ilikuwa na nguvu zaidi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo alipokutana na kundi la washairi na wasomaji kaswida za kuwasifia Ahlul-Beiti (as) kwa mnasaba wa kuwadia maadhimisho ya kuzaliwa Bibi Fatma Zahra (SA) binti mtukufu wa Bwana Mtume (SAW) na kusisitiza kwamba, mpango jumla wa adui umefeli kwa sababu alikosea katika mahesabu yake.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuwa na mapenzi na Bibi Fatma (SA) ni jambo lenye taathira katika masuala ya mtu binafsi na yasiyo ya binafsi na kueleza kwamba, wasomaji mashairi na kaswida za kuwasifu Ahlul-Beit (AS) ni turathi ya Ushia na ni Sanaa ambayo inaundwa na sauti nzuri na mashairi ya kuvutia.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, adui alitumia nyenzo zote kwa ajili ya kutia dosari na kukwamisha mambo hapa nchini na kuongeza kuwa, kupenyeza timu za kijasusi, makelele na propaganda za kuchafua jina la Iran na kulionyesha taifa hili kuwa ni tishio na propaganda mbalimbali ni miongonii mwa mambo yaliyotumiwa na adui katika miezi ya hivi karibuni hapa nchini.

Hata hivyo Ayatulllah Khamenei ameeleza kuwa, maadui wameshindwa kufikia malengo yao kwani mahesabu yao hayakuwa sahihi.

Kiongozi Muadhamu ameongeza, maadui walikuwa wakidhani kwamba, wananchi wa Iran kutokana na matatizo ya kiuchumi wanayokabiliwa nayo watakuwa pamoja nao katika mpango wao wa kuuangusha mfumo na takwa lao la kuigawa nchi hii.

Kadhalika amesema, walikuwa wakidhani kwamba, kwa kutoa matusi na maneno machafu na udhalilishaji wataweza kuwatoa viongozi wa mfumo katika medani au kwa kufanya uchochezi wanaweza kuzusha hitilafu za kimitazamo baina ya viongozi wa ngazi za juu na walikuwa wakidhani kwamba, kwa dola za mafuta za nchi fulani na ufujaji wa fedha dhidi ya Iran, vijana wetu watakata tamaa, walikosea, kwani vijana waliwapuuza.

4114069

captcha