IQNA

Wasiwasi wa Waislamu Italia baada muungano wa mrengo wa kulia kuchukua madaraka

22:32 - September 26, 2018
Habari ID: 3471692
TEHRAN (IQNA)- Hofu imetanda miongoni mwa Waislamu nchini Italia baada ya serikali yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia kuchukua madaraka nchini humo.

Katika mahojiano na Televisheni ya Al Jazeera, Yassine Lafram, Mwenyekiti wa Muungano wa Jamii za Waislamu Italia (UCOII) amebaini kuwa chuki za wazi dhidi ya Waislamu na wahajiri nchini humo zimeshika kasi kuanzia mitandao ya kijamii hadi mitaani.
Amesema ni jambo la kusikitisha kuwaona wanasiasa wakitoa kauli za kuchochea chuki dhidi ya wahajiri na jamii ya Waislamu nchini humo na yumkini matamshi hayo yakabadilika na kuwa vitendo katika siku sijazo.
Waislamu nchini Italia wanaishi kwa wasiwasi mkubwa kutokana na kushtadi vitendo vya chuki na mashambulizi yanayosukumwa na hisia kali zilizo dhidi ya dini yao.
Mohamed Ben Mohamed, Imam wa Msikiti wa Centocelle amesema jamii za Waislamu nchini humo zinaishi kwa hofu kubwa, na wasiwasi huo umeongezeka maradufu kwani hawajui serikali hii mpya inawapangia nini.
Katika kipindi cha kampeni, Matteo Salvini, Waziri wa Mambo ya Ndani wa sasa alitishia kuifunga misikiti yote nchini humo na kutoruhusu ujenzi wa misikiti mipya, akidai kuwa Uislamu hauendani na katiba ya nchi hiyo.
Kuna Waislamu milioni 2.6 nchini Italia, sawa na asilimia 4 ya idadi jumla ya watu wa nchi hiyo.
Uchunguzi wa maoni uliochapishwa Septemba mwaka jana na Idara ya Haki za Kimsingi ya Umoja wa Ulaya (EU Fundamental Rights Agency) ulibaini kuwa Waislamu barani Ulaya wanahisi kuongezeka ubaguzi ambapo wawili kati ya watano (asilimia 40) wakisema wamekumbana na ubaguzi wakati wa kutafuta kazi, nyumba au huduma za umma kama vile elimu an matibabu.
Ripoti hiyo ilisema Waislamu ni karibu asilimia 4 ya watu wote barani humo na kwamba asilimia 78 wanasema wanaufungamano wa kizalendo na nchi wanamoishi huku asilimia 92 wakisema hawana tatizo kuishi na majirani wasio Waislamu. Baadhi ya duru zinasema idadi ya Waislamu barani Ulaya ni asilimia 7.66 au watu milioni 56 kati ya watu takribani milioni 740 barani humo.

3466842

captcha