IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iwapo hatua ya kimantiki itachukuliwa, inawezekana kusambaratisha mahesabu ya adui

21:02 - April 16, 2023
Habari ID: 3476877
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa iwapo hatua za kimantiki zitachukuliwa, inawezekana kushindwa mahesabu ya adui

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo Jumapili katika kikao chake na makamanda na maafisa wakuu wa Jeshi la Iran ambapo amevitaja vikosi vya jeshi hilo kuwa ni ngome imara za nchi na taifa kama alivyosema Amirul Muuminina Ali bin Abi Talib AS). Amesisitiza kuwa: "Nafasi hii ya juu inaandamana na majukumu mazito, na ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba, vikosi vya jeshi vinathamini nafasi hiyo yenye fahari kubwa na vinatekeleza majukumu yao."

Akielezea kuridhishwa kwake na harakati na maendeleo endelevu katika vikosi vya jeshi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Msiridhike na nguvu na maendeleo yaliyopatikana hata kidogo, na endeleeni kusonga mbele bila kusita.

Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran ameashiria Aya ya Qur'ani Tukufu akisema, kuwa tayari wakati wote ni jambo lililoamrishwa na Mwenyezi Mungu na chanzo cha kuwatia hofu maadui wa Mwenyezi Mungu na taifa na kuongeza kuwa: Tishio la adui halijatoweka kamwe, hivyo basi mnapaswa kuongeza utayarifu wenu kadiri muwezavyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ametaja utayarifu wa vikosi vya jeshi kwa ajili ya kukabiliana na maadui kuwa ni kinga ya taifa; na kwamba kuwa macho mkabala wa wale wanaopanga njama za nyuma ya pazia ni jambo lenye muhimu mkubwa.

Akizungumzia uchochezi wa vikosi viovu vya kimataifa katika maeneo tofauti ya dunia, Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Iran amesema: Mabeberu huanzisha mapigano na mizozo kutokea nyuma ya pazia popote wanapoona maslahi yao.

Nukta nyingine muhimu iliyosisitizwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa makamanda na maafisa wakuu wa jeshi ni kuzingatia na kuwa makini mbele ya mipango ya muda mrefu ya adui. Katika muktadha huo Ayatullah Khamenei amesema: Ni vyema na ni lazima kutilia maanani sana mipango ya adui ya miaka mitano au kumi, lakini mipango yake ya kati na ya muda mrefu inapaswa kutiliwa maanani na kufuatiliwa.

Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Iran ameashiria vita viwili ambavyo Marekani ilianzisha Mashariki na Magharibi mwa Iran takriban miongo miwili iliyopita, na kusema: Wamarekani walikuwa na maslahi huko Iraq na Afghanistan, lakini lengo lao kuu lilikuwa Iran ya Kiislamu, hata hivyo kutokana na msingi imara wa Mapinduzi ya Kiislamu, walishindwa kufikia lengo lao kuu.

Ameitaja hali ya hivi sasa ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni mfano mwingine wa kushindwa huko na kusema: Mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika mwezi wa Ramadhani mwaka jana hayakukabiliwa na radiamali mahususi duniani, lakini mwaka huu uhalifu na jinai zake zimekabiliwa na maandamano katika nchi mbalimbali duniani hata huko Marekani na Uingereza.

Amiri Jeshi Mkuu wa Iran amesema ni muhimu sana kutompuuza adui pamoja na kuamini kwamba adui anaweza kushindwa, na kuongeza kuwa: Hatupasi kufumbia macho hata kidogo njama na mipango ya adui.

4134578

4134578

captcha