IQNA

Watetezi wa Palestina

Hizbullah yatangaza kushambulia maeneo ya kijeshi ya Israel kuunga mkono Gaza

18:19 - December 17, 2023
Habari ID: 3478048
IQNA-Wapiganaji wa harakati ya Mapambano ya Kiislamu (muqawama) ya Hizbullah ya Lebanon wameendelea na mashambulizi yao dhidi ya ngome za kijeshi la utawala haramu Israel karibu na mpaka kati ya Lebanon na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), kujibu vita vya utawala huo haramu wa Israel dhidi Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Taarifa ya Hizbullah iliyotolewa Jumapili, imebaini kuwa kundi hilo limewalenga wanajeshi wa utawala dhalimu wa  Israel kwenye kambi ya Birkat Risha, na kusababisha hasara miongoni mwa wanajeshi vamizi.

Aidha wanajeshi kadhaa wa Israel pia walijeruhiwa, wakati wa mashambulizi zaidi ya Hizbullah karibu na kituo cha kijeshi cha Hanita, kilichoko takriban kilomita 15 (maili 9.3) kaskazini mashariki mwa Nahariya.

Hizbullah ilisema Jumamosi kwamba iliendesha mashambulizi mawili kwenye kituo cha Israel cha Birkat Risha karibu na mpaka, na kusababisha vifo na majeruhi.

Ripoti za vyombo vya habari zilisema wanajeshi wanne wa Israel walijeruhiwa katika mashambulizi hayo, mmoja wao akiwa mahututi.

Hizbullah baadaye ilitangaza kushambulia vituo vinne zaidi vya Israel, ikisema ililenga makundi ya wanajeshi wa Israel.

Huku hayo yakijiri, mashambulizi ya makombora ya Israel yalilenga eneo la Wadi Hassan nje kidogo ya mji wa mpakani wa Lebanon wa al-Jibbain pamoja na viunga vya miji ya Lebanon ya Khiam, Deir Mimas, Blida, Houla, Mays al-Jabal na Kfarkila.

Hizbullah katika taarifa yake ilitangaza kifo cha mpiganaji wake mmoja zaidi, aliyetambuliwa kama Radwan Hammoudi, ikisema anatokea mji wa kusini wa Tiro.

Baadaye siku ya Jumamosi, vyombo vya habari vya Israel viliripoti ving'ora vya tahadhari katika sehemu ya kaskazini ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu (Israel) na milipuko katika eneo la Upper Galilee.

Utawala wa Israel umekuwa ukifanya mashambulizi ya hapa na pale kusini mwa Lebanon tangu Oktoba 7, ulipoanzisha vita vya kutisha dhidi ya Ukanda wa Gaza unaozingirwa.

Hizbullah hutekeleza mashambulizi ya roketi karibu kila siku kwenye maeneo kwenye mpaka huku Israel ikitekeleza mashambulizi ya angani na mizinga kusini mwa Lebanon.

Zaidi ya watu 120 wameuawa katika upande wa mpaka wa Lebanon tangu Oktoba 7, wengi wao wakiwa wapiganaji wa Hizbulah na zaidi ya raia kumi na wawili.

Israel inasema takriban wanajeshi wake sita na walowezi wanne wameuawa katika eneo hilo, na jeshi la Lebanon lilipoteza mwanajeshi mmoja.

Raia kumi na saba wa Lebanon, watatu kati yao waandishi wa habari, pia wamepoteza maisha katika mabadilishano hayo.

4188433

Habari zinazohusiana
captcha