IQNA

Utawala wa Israel wawazuia Wapalestina kusali katika Msikiti wa Nabii Ibrahim AS

18:13 - October 31, 2021
Habari ID: 3474497
TEHRAN (IQNA) Kwa mara nyingine, Utawala wa Kizayuni wa Israel unawazuia Waislamu Wapalestina kuingia Msikiti wa Nabii Ibrahim AS katika mji wa Al Khalil (Hebron) ulio katika eneo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, linalokaliwa kabavu na utawala huo ghasibu.

Mkurugenzi wa msikiti huo Sheikh Hefzy Abu Asinina amenukuliwa akisema utawala haramu wa Israel sasa unawaruhusu tu walowezi wa Kizayuni kuingia katika eneo hilo takatifu kwa ajili ya ibada ya Kiyahudi ijulikanayo kama Chayei Sarah.

"Msikiti ulifungwa Ijumaa saatisa mchana hadi Jumamosi saa nne usiku," amesema Abu Asinina. Wakati wa ibada za Kiyahudi, jeshi la utawala haramu wa Israel huwazuia Waislamu kuingia katika msikiti katika kipindi cha hadi siku 10 kwa mwaka.

Msikiti wa Ibrahim AS ambao ni eneo takatifu kwa Waislamu na Mayahudi  ni Haram Takatifu na uko katika kitongoji cha kale cha Al Khalil (Hebron) kusini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, ndani ya msikiti huo kuna kaburi la Nabii Ibrahim AS na mkewe Sarah na vile vile makaburi ya Manabii Is-haq na Yaaqub AS na ya wake zao.

Itakumbukuwa kuwa mnamo mwezi Julai mwaka 2017, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza kuwa mji wa Al Khalil ulioko Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan ambao ni moja ya turathi za kimataifa unakabiliwa na hatari kutokana na sera haribifu za utawala wa Kizayuni.

3476267

captcha