IQNA

Ulimwengu wa Kiislamu

Kiongozi Muadhamu: Masaibu ya Gaza ni ya wanadamu na yanaonyesha mfumo wa sasa ulimwenguni ni wa batili

18:58 - February 08, 2024
Habari ID: 3478321
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumza kuhusu tukio chungu na la kuhuzunisha la Gaza na kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni, na akasema: “masaibu ya Gaza ni masaibu ya wanadamu na yanaonyesha kuwa utaratibu wa sasa wa ulimwengu ni wa batili tupu, usioweza kudumu na utatoweka tu.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo jijini Tehran katika mkutano na viongozi na watendaji wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, mabalozi na wawakilishi wa nchi za Kiislamu pamoja na wananchi wa matabaka tofauti uliofanyika kwa mnasaba wa kuadhimisha Idi ya Mab'ath ya kupewa Utume Nabii Muhammad Al Mustafa SAW.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa: "leo Marekani, Uingereza na nchi nyingi za Ulaya pamoja na wafuasi wao, wako nyuma ya jinai zinazofanywa na mikono iliyotapakaa damu ya utawala wa Kizayuni, na ndipo tunapoweza kufahamu kwamba, mfumo wa sasa wa dunia ni wa batili, usioweza kudumu na utatoweka tu".
 
Ameyaelezea pia mashambulio ya mabomu na makombora yanayolenga hospitali na kuuliwa karibu watu 30,000 huko Gaza kuwa ni fedheha kwa utamaduni na ustaarabu wa Magharibi na akaongeza kuwa: "nyuma ya jinai hizi kuna fedha, silaha na misaada ya kisiasa ya Marekani; na kama Wazayuni wenyewe walivyokiri kwamba wasingeweza kuendeleza vita hata kwa siku moja bila ya silaha za Marekani, kwa hiyo Wamarekani pia wana hatia na wanabeba dhima ya tukio hili chungu".

Ayatullah Khamenei amesema, suluhisho la kuhitimisha mgogoro wa Gaza ni kujiondoa madola makubwa ya Magharibi na wafuasi wao katika kadhia hiyo na akabainisha kuwa: wanamapambano wa Palestina wanao uwezo wa kuendeleza mapambano, kama ambavyo hadi sasa wanafanya hivyo, na wala hawajapata pigo kubwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, wajibu wa serikali ni kukata misaada ya kisiasa, kipropaganda na ya silaha na kuacha kuipelekea bidhaa za matumizi utawala wa Kizayuni; na akakumbusha kuwa: jukumu la wananchi wa mataifa ni kuzishinikiza serikali zao ili zitekeleze jukumu hilo kubwa.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amesema kufanikiwa kwa Mapinduzi ya Kiislamu ni matunda na matokeo ya kuitikiwa na wananchi wito wa ujumbe wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na wito wa Imamu Khomeini (MA), na akaongeza kuwa: baada ya hapo, kwa taufiki na fadhila za Mwenyezi Mwenyezi Mungu wananchi wa Iran wameendelea kusonga mbele kwa kufuata njia iliyo sawa; na kila watakapoendelea kuitikia wito wa Mtume SAW watapata ustawi na maendeleo, si kwa upande wa kiroho tu na kwa ajili ya akhera pekee, bali pia kwa kuwa na mfano bora wa maisha ya duniani na akhera. 
 
Ayatullah Khamenei ameashiria kuenea kwa dhulma na utovu wa haki katika ulimwengu wa leo na akasema, kuondokana na hali hiyo na kuboresha maisha ya watu duniani kumefungamana na kuitikia wito wa Bwana Mtume SAW na kutumia muongozo wa kuzitakasa nafsi na mafundisho ya Utume; na akafafanua kwamba: "wajibu wetu sisi ni kuzijenga nafsi zetu na kuonesha uendeshaji wa Iran kuwa unafuata kigezo cha Uislamu, ambapo katika hili, tumepata mafanikio kadhaa ambayo yamekuwa na taathira ulimwenguni, lakini bila shaka tumekuwa na mapungufu pia".
 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amewatakia kheri na baraka wananchi wa Iran na Waislamu wote kwa mnasaba wa Idi ya Kupewa Utume Nabii Muhammad SAW na akasema, Mab'ath ni tukio la baraka zaidi na kubwa zaidi lililotokea katika historia ya mwanadamu na akaongezea kwa kusema: kwa kubaathiwa Mtume Mtukufu, toleo lililokamilika, la mwisho na la milele la saada na fanaka ya mwanadamu duniani na akhera lilifikishwa kwa watu.

4198731

captcha