IQNA

Mwanamke ateuliwa kwa mara ya kwanza kuwa waziri mkuu Tunisia

20:46 - September 29, 2021
Habari ID: 3474359
TEHRAN (IQNA)- Rais Kais Saied wa Tunisia amemetua Najla Bouden Romdhane, kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi hiyo, baada ya kupita takribani miezi miwili tangu alipohodhi madaraka yote ya nchi, hatua iliyoelezwa na wapinzani wake kama mapinduzi ya kijeshi.

Bi Bouden, ambaye ni mhandisi wa chuo kikuu asiye na umaarufu, aliyewahi pia kuhudumu katika Benki ya Dunia anashika wadhifa huo mpya wa uwaziri mkuu wakati Tunisia imegubikwa na wingu zito la mgogoro wa kitaifa, ambao umeyatia mashakani mafanikio ya kidemokrasia yaliyopatikana kupitia mapinduzi ya umma ya mwaka 2011.

Mnamo mwezi Julai, Rais Kais Saied alimuuzulu waziri mkuu, akalisimamisha bunge na kuhodhi madaraka yote ya utendaji. Tangu wakati huo amekuwa akishinikizwa ndani ya nchi na kimataifa aunde serikali mpya.

Mnamo wiki iliyopita, kiongozi huyo alipuuzilia mbali ulazima wa kuendesha nchi kikatiba na kusema kuwa anaweza kuongoza kwa kutumia zaidi dikrii za urais.

Ofisi ya rais wa Tunisia imetangaza kupitia mitandao ya kijamii kuwa, Rais Saied ametumia sheria za muda alizotangaza wiki iliyopita kumteua Bi Najla Bouden Romdhane kuwa waziri mkuu na kumtaka aunde serikali haraka.

Rais wa Tunisia amesema, jukumu la serikali mpya litakuwa ni kukomesha ufisadi na ufanyaji mambo ndivyosivyo ulioenea katika taasisi nyingi za dola.

Dakta Bouden, mwenye umri wa miaka 63 kama alivyo Rais Saied, anakuwa waziri mkuu wa 11 wa Tunisia tangu mapinduzi ya mwaka 2011 yaliyohitimisha utawala wa kidikteta wa  Zine El Abedine Ben Ali na kuchochea kile kilichojulikana kama Machipuo ya Kiarabu.

3475844

captcha