IQNA

Iran na Afrika

Iran yapongeza azma ya Mali ya kukabiliana na ugaidi

14:57 - August 24, 2022
Habari ID: 3475671
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyeko safarini Bamako mji mkuu wa Mali ameipongeza nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kwa juhudi zake kubwa za kupambana na makundi ya kigaidi.

Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake na Kanali Assimi Goita, Kiongozi wa serikali ya mpito ya Mali na kutoa mwito wa kuimarishwa zaidi ushirikiano wa kiuchumi, kibiashara na kielimu baina ya nchi mbili hizi.

Sambamba na kubainisha tajiriba ya Iran katika kupambana na makundi ya kigaidi kama Daesh au ISIS, Hussein Amir-Abdollahian amesema kuwa, taifa la Iran licha ya kuandamwa na vikwazo vya kiuchumi vya kidhalimu, lakini limeweza kulinda njia yake endelevu katika kulinda mamlaka ya kisiasa na maendeleo yake ya kiuchumi na kielimu.

Kwa upande wake Kanali Assimi Goita, Kiongozi wa Serikali ya Mpito ya Mali ametaka kuimarishwa zaidi ushirikiano wa Bamako na Tehran katika nyuga za kiuchumi, kibiashara na kielimu na kueleza utayari wa nchi yake wa kuwa mwenyeji wa wenye viwanda na wanaharakati wa kiuchhumi.

Aidha amesema mafanikio ya taifa la Iran katika kukabiliana na vikwazo vya kidhalimu na kupata nafasi muhimu ya kisiasa na kiuchumi katika uga wa kieneo na kimataifa ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine ambayo yanakabiliana na uingiliaji wa madola ajinabi.

Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatatu ya jana aliondoka hapa mjini Tehran na kuelekea Bamako mji mkuu wa Mali, hii ikiwa ni safarii yake ya kwanza barani Afrika tangu alipoteuliwa kuchukua wadhifa huo.

Safari hii inafanyika kujibu mwaliko wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Mali. Ujumbe wa kisiasa na kiuchumi pamoja na baadhi ya wafanyabiashara wa sekta binafsi nchini Iran wameandamana na Abdollahian katika safari yake hiyo. Baada ya kukamilisha safari yake nchini Mali, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran anatarajiwa kuelekea nchini Tanzania. Aidha anatarajiwa kuvitembelea pia visiwa vya Zanzibar ambavyo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

https://mfa.gov.ir/portal/NewsView/691012

captcha