IQNA

Brigedia Jenerali Mohammad Baqeri

Hakuna dola linalothubutu kuanzisha uadui na uchokozi dhidi ya Iran

21:30 - December 14, 2021
Habari ID: 3474675
TEHRAN (IQNA)- Mkuu wa Kamandi ya vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, "hatujaghafilika hata kwa lahadha na sekunde moja kustawisha uwezo wa kiulinzi na nguvu za kijeshi za kuzuia hujuma dhidi ya nchi."

Brigedia Jenerali Mohammad Baqeri ameyasema hayo leo katika semina ya mabalozi na wakuu wa ofisi za uwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi jirani na akabainisha kuwa, vikwazo na mashinikizo vimepelekea mkabala wake kujengeka moyo wa kusimama kidete, kuwa imara, kujitegemea, kujiamini na kujizatiti kwa hima na juhudi kubwa mfumo mzima wa ulinzi nchini.

Brigedia Jenerali Baqeri ameongezea kwa kusema: katika kuukabili na kuutolea jibu uadui wa kimataifa unaofanywa dhidi ya Iran, hatua kadhaa za kistratejia zimepewa kipaumbele katika uga wa ulinzi nchini; na kwa baraka za damu za mashahidi na tadbiri na miongozo ya hekima ya Imam Khomeini (MA) na baada yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, sekta ya ulinzi ya nchi imefikia upeo wa ustawi na utukukaji na kuweza kuzuia hujuma, kiasi kwamba leo hii hakuna dola linalothubutu kuanzisha uadui na uchokozi dhidi ya Iran. 

Kamanda wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, katika kukabiliana na adui, vikosi vya ulinzi havijawahi kupuuza na kudogosha kitisho chochote kile, kwa sababu katika uga wa stratejia ya utayarifu na kuwa macho imejiandaa kwa kiwango cha juu kukabiliana kitisho cha kiwango cha chini kulingana na adui alivyo.

Brigedia Jenerali Baqeri amekumbusha pia kuwa, kile kilichoshuhudiwa na walimwengu hivi karibuni, likiwemo shambulio dhidi ya kituo cha jeshi la kigaidi la Marekani cha Ainul-Asad na kutunguliwa ndege isiyo na rubani ya kisasa kabisa ya jeshi hilo katika eneo la majini la Iran kwa kutumia mitambo ya ulinzi wa anga iliyoundwa nchini, ni funzo na ibra ya kutoa mazingatio hasa kwa maadui hao wafanyao chokochoko.

4020865

Kishikizo: iran baqeri jeshi
captcha