IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Raia wa Iran waungana katika kutia saini Ombi 'Kubwa Zaidi' la kupinga kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu

20:57 - September 18, 2023
Habari ID: 3477619
TEHRAN (IQNA) - Raia wa Iran wameungana katika kutia saini ombi "kubwa zaidi" la kupinga kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu baada ya kurudiwa kwa vitendo kudhalilisha Kitabu Hicho Kitukufu cha Waislamu katika nchi za Magharibi.

Kiasi cha mita 250 za ombi hilo hivi sasa zimeonyeshwa katika miji mitakatifu ya Iran ya Qom na Mashahd.

Ombi hilo lina urefu wa mita 1,114, na asilimia 80 yake ilionyeshwa nchini Iraq wakati wa maombolezo ya Siku ya Arbaeen ya Imam Hussein (AS) ili wafanyaziayar waliofika kutoka duniani kote waweze kutia saini.

Arbaeen huadhimisha siku ya 40 iliyofuata kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), Mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imam wa tatu wa Shia,  ambaye aliuawa shahidi akiwa na masahaba zake 72 katika Vita vya Karbala, katika eneo ambalo sasa ni kusini mwa Iraq, mwaka 680 Miladia. Imam Hussein (AS) alikuwa amesima kupinga dhulma iliyokuwa ikitekelezwa na watawala wa wakati huo.

Kila mwaka, mamilioni ya waombolezaji wa Kiislamu huingia katika matembezi ya mfano ya urefu wa kilomita 80 yanayoanzia mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq, ambako ndiko alikozikwa babake Imam Hussein, Imam Ali (AS) hadi mji mtakatifu wa Karbala ambako amezikwa Imam Hussein (AS).

Ombi hilo lilianzishwa na Kambi ya Qur'ani ya Arbaeen ambayo ilitoa tamko la kulaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika lugha nne za Kiajemi, Kiarabu, Kiurdu na Kiingereza.

Ombi hilo ni sehemu ya hatua za kivitendo na madhubuti zinazolenga kuzuia vitendo vya unajisi vitabu vitakatifu na matakatifu.

Matukio kadhaa yametokea katika miezi ya hivi karibuni ambayo yalionyesha kuvunjiwa heshima kwa Qur'ani Tukufu huko Denmark na Uswidi kwa idhini ya mamlaka ya nchi hizo mbili.

Vitendo hivyo vya kufuru vimelaaniwa vikali duniani kote na pia kukabiliwa na maandamano katika ulimwengu wa Kiislamu, ikiwemo Iran, huku nchi zote za Kiislamu zikilaani vikali.

Hivi sasa, mita 150 ombi hilo zimeonyeshwa katika yadi ya Haram Tukufu ya Imam Ridha (AS) mjini Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran mita 100 zake ziko katika yadi ya Haram Takatifu ya Fatemeh Masumeh (SA) mjini Qum kusini mwa Tehran ili wafanyaziyara  waweze kutia saini.

Hayo yalijiri wakati mamilioni ya waombolezaji walikuwa  wamekusanyika katika Mashhad ya Mkoa wa Khorasan wa Razavi katika kumbukizi ya kuuawa shahidi Imam Ali bin Musa al-Ridha (AS) mnamo Septemba 16 mwaka huu.

Hojjat Ganadabi, afisa katika jimbo hilo alisema Jumamosi kwamba zaidi ya wafanyaziara milioni 4.5 waliingia Mashhad katika kipindi cha siku 10.

Habari zinazohusiana
Kishikizo: watetezi wa qurani
captcha